Thursday, 11 June 2015

Ngo Ngonedo's blog: MAONI: Leo ni Bajeti, ni muhimu kuisikiliza, kuielewa

www.ngonedo.org
Watanzania leo wanaelekeza macho na masikio yao mjini Dodoma,
kusikiliza Hotuba ya Bajeti ya Serikali, inayotarajiwa kusomwa saa 10
jioni bungeni na Waziri wa Fedha, Saada Mkuya.
Tayari Waziri Saada alishaeleza kuwa bajeti ya
mwaka wa fedha wa 2015/16, inatarajiwa kuwa ya Sh22.480 trilioni, kwa
matumizi ya kawaida na maendeleo. Ni jambo lililo wazi kwamba bajeti ni
mpango au mkataba wa namna Serikali itakavyokusanya na kutumia fedha za
wananchi.
Jambo muhimu katika bajeti ni namna Serikali
inavyotumia fedha katika vipaumbele na mipango mbalimbali. Tunafahamu
kuwa bajeti huandaliwa na kutekelezwa kwa kipindi cha mwaka wa fedha,
badala ya mwaka wa kalenda. Kwa Tanzania, mwaka wa fedha huanzia Julai
hadi Juni 30 wa mwaka unaofuata. Mchakato wa bajeti ni mzunguko
unaoendelea mwaka mzima.
Bajeti inahusu fedha au rasilimali za wananchi,
kwa hiyo inatupatia dirisha la kufahamu umakini wa kweli wa Serikali
katika utatuzi wa matatizo mbalimbali ya wananchi katika juhudi za
kuleta maendeleo.
Hivyo basi ushiriki wa wananchi kuanzia mchakato
hadi katika mjadala bungeni kupitia wawakilishi wao, utaboresha
uwajibikaji, kuzuia fursa za rushwa na kusimamia matumizi endelevu ya
rasilimali za umma na hatimaye kusaidia kuondoa matatizo yanayoikabili
jamii ikiwamo umaskini.
Kwa upande mwingine, wananchi wana umuhimu mkubwa
katika suala la bajeti, kwani mamlaka yote ya Serikali na viongozi wa
umma hutoka kwa wananchi. Hii ina maana kuwa wananchi ndiyo wenye
mamlaka makubwa zaidi ambayo hutoa uhalali na mamlaka kwa Serikali na
vyombo vyake.
Vivyo hivyo, rasilimali zote za Taifa na ugawaji
wake kimatumizi, vinakuwa chini ya wananchi. Wananchi ndiyo wanaolipa
kodi na kutoa michango mbalimbali inayoiwezesha Serikali kutekeleza
mipango ya maendeleo.
Kwa mantiki hiyo, wananchi ndiyo wenye masilahi na
rasilimali zao, kwa mustakabali wa nchi yao, hivyo shauku ya kushiriki
suala la bajeti na utekelezaji wake, ni suala la msingi kwa kila
mwananchi kulizingatia.
Takwimu zinaonyesha kuwa karibu asilimia 80 ya
wananchi wote wa Tanzania ni wakulima, wafugaji wadogo na wa kati. Hivyo
ni muhimu kwa kundi hili kuzingatia mamlaka yake na kushiriki
kikamilifu katika kuisikiliza na kuielewa bajeti itakayowasilishwa
bungeni leo na Waziri Mkuya.
Hatua hiyo itawasaidia kuilewa kwa kusikiliza wenyewe badala ya kuhadithiwa, kuichambua na kuitathmini kwa mapana na marefu.
Huu ni mwaka wenye mambo mengi ya kitaifa, mbali
na shughuli za maendeleo, pia kuna uandikishaji wa Daftari la Kudumu la
Wapigakura, vitambulisho vya Taifa na Uchaguzi Mkuu, mambo yote hayo
yanahitaji kujadiliwa kwa umakini, lakini mjadala wenye afya utatokana
na usikilizaji makini wa hotuba ya bajeti.
Usilikizaji wa bajeti ni njia ya kumuongezea
uwelewa mwananchi wa kawaida, kujua katika eneo lake kuna mipango ipi ya
maendeleo na imetengewa kiasi gani ili waweze kuhoji kwenye mikutano,
mfano, Kamati za Maendeleo ya Kata (WDC), mikutano ya maendeleo ya jimbo
na vilevile, katika halmashauri zao.



Lakini pia ndani ya Bunge, kumekuwa na lawama kwamba mijadala ya
bajeti mara nyingi hujikita katika ushabiki wa kisiasa, kupigana
vijembe na hata Bajeti Mbadala ya Kambi Rasmi ya Upinzani, huzodolewa
kwamba ni ‘bajeti ya harusi’ na kauli nyingine nyingi za kejeli.
Bajeti hii ambayo ni ya mwisho kwa utawala wa Rais
Jakaya Kikwete ni vyema ikawa mfano kwa kusikilizwa kwa umakini na
kujadiliwa kwa hoja, pia kwa ni jambo la muhimu kwa wabunge kutulia
bungeni hadi wakati wa kuipitisha, kwa kujenga hoja na kuwasaidia
wananchi kuielewa wakati wa mjadala.